Mashindano ya 3 ya Dunia ya Mbio za Nusu Marathoni za Majeshi (3rd CISM World Military Half Marathon Championship) yanatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 3 hadi 7 Aprili 2026 katika jiji la Antalya nchini Uturuki, yakiwakutanisha wanamichezo wa majeshi kutoka mataifa mbalimbali duniani. Mashindano hayo yanaandaliwa na International Military Sports Council (CISM), yenye lengo la kuimarisha mshikamano, ushindani wa kirafiki pamoja na kukuza vipaji vya michezo miongoni mwa wanajeshi.
Katika habari picha, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania, Brigedia Jenerali Saidi Hamis Saidi (katikati), akiwa pamoja na Luteni Kanali Penina Igwe (wa kwanza Kulia), wanaonekana sambamba na wanariadha wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakiwa nchini Uturuki tayari kwa ushiriki wao katika mashindano hayo. Uwepo wao unaashiria dhamira ya dhati ya Tanzania kushiriki kikamilifu katika mashindano ya kimataifa ya kijeshi.
Timu ya wanariadha ya JWTZ imewasili ikiwa na maandalizi ya kutosha na morali ya juu, wakilenga kufanya vizuri na kuiwakilisha vyema Tanzania. Ushiriki wao unatarajiwa kuongeza ushindani katika mashindano hayo, huku ukiendelea kudhihirisha mchango wa michezo katika kuimarisha mahusiano ya kimataifa miongoni mwa majeshi duniani.
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania Brigedia Jenerali Saidi Hamis Saidi (katikati) na Luteni Kanali Penina Igwe (wa kwanza kulia) wakiwa na Wanariadha kutoka JWTZ nchini Uturuki.