KUHUSU BAMMATA
Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) ni chombo cha kitaalamu cha michezo kilichosajiliwa kihalali kwa lengo la kusimamia na kuratibu shughuli za michezo kwa Vyombo vya Ulinzi, Usalama na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).Baraza hili lilianzishwa rasmi mwaka 1977, Likijumuisha kanda nane ambazo ni Kanda ya Ngome, kanda ya JKT, Kanda ya Polisi, Kanda ya Magereza, Kanda ya Uhamiaji, Kanda ya Zimamoto, Kanda ya Visiwani na Kanda ya SMZ
UTANGULIZI
Michezo ni sehemu muhimu sana katika utamaduni kila jamii ya binadamu duniani kote. Majeshi ya ulinzi na usalama kama jamii yamekuwa yakishiriki katika michezo mbalimbali kwa lengo la ;
(1) Kujenga na kukomboa afya ya mwili na akili kwa maafisa na wapiganaji;
(2) Kujenga tabia ya ushirikiano, upendo, undugu na uzalendo miongoni mwa wanajeshi na jamii;
(3) Kujenga moyo wa kishujaa, ujasiri, ukakamavu na kujiamini;
(4) Kutoa burudani kwa wapiganaji, wananchi na jamii kwa ujumla ili kuiepusha na muda wa kutenda mambo maovu;
(5) Kuimarisha mahusiano baina ya wapiganaji, maafisa na jamii;
(6) Kujenga ukakamavu, nidhamu na uwezo wa kujiamini kwa wapiganaji;
(7) Kuonesha uwezo na vipaji vya askari, kukuza uhusiano wa kirafiki baina ya askari.
Baada ya uhuru mwaka 1967 lilianzishwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa sheria namba 12 ambalo lina jukumu la kuongoza na kuratibu maendeleo ya michezo kwa kushirikiana na mabaraza ya vyama vya michezo.
Tangazo la serikali Na. 471 la tarehe 16 Novemba, 1990 limeruhusu kuanzishwa kwa mabaraza ya michezo ambayo shughuli zake zimeorodheshwa chini ya Baraza la Michezo la Taifa (5.1.3) (a)-(i).
Pamoja na sababu nyingine, kwa kuzingatia tanganzo hilo Majeshi ya Ulinzi na Usalama ambayo kila moja lilikuwa linafanya michezo yake yakaona kuna umuhimu kuwa na Baraza la Michezo la Majeshi (BAMMATA) kama chombo muhimu ambacho kitafanya yafuatayo-
(1) Kutoa ushauri wa kitaalamu katika harakati za kuendeleza michezo ya majeshi;
(2) Kuweka utaratibu wa uhusiano katika kuendeleza michezo baina ya majeshi yetu;
(3) Kuweka mipango dhabiti ya kuendeleza michezo kwa majeshi wanachama;
(4) Kuhakikisha kuwa kuna watalamu wa michezo na wanamichezo katika majeshi wanachama
BAMMATA ni muhimili mkuu wa michezo kwa majeshi wanachama siyo tu katika ulinzi bali kuyaweka pamoja, kuyaunganisha na jamii na zaidi sana kuchangia kukuza michezo kwa Taifa
SURA YA KWANZA
JINA, ANUANI, MAKAO MAKUU, USAJILI, DHIMA NA DIRA
1. JINA
Jina litakuwa "BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI TANZANIA" kwa kifupi BAMMATA
2. ANUANI
Anuani ya ofisi ya BAMMATA itakuwa ni;
Ofisi ya BAMMATA,
Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania,
S.L.P 194,
DODOMA, TANZANIA.
3. MAKAO MAKUU
Makao Makuu ya BAMMATA yatakuwa yalipo Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania au sehemu yoyote itakayoamuliwa.
4. USAJILI
BAMMATA imesajiliwa chini ya Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa ya Mwaka 1967 kama ilivyofanyiwa marekebisho Mwaka 2018.
5. DHIMA
Kudumisha michezo ya vyombo vya Ulinzi na Usalama na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ili viwe vitalu vya maendeleo ya michezo nchini.
6. DIRA
Kuwa chombo cha kuhakikisha ushiriki endelevu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama na Idara Maalum za SMZ katika michezo ya kimashindano ndani na nje ya nchi ili kuinua viwango kwa kuwa na walimu na wanamichezo wanaoweza kuliwakilisha Taifa na kuhakikisha wanachama wanakuwa na vifaa na viwanja bora ili kudumisha utimamu wa mwili na akili.
SURA YA PILI
MADHUMUNI
Madhumuni ya Baraza ni yafuatavyo:-
1. Kulinda na kutunza heshima ya vyombo vya Ulinzi na Usalama na Idara Maalum za SMZ katika taswira ya michezo;
2. Kuendeleza uhusiano, urafiki na undugu baina ya Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Idara Maalumzya SMZ na Wananchi kwa ujumla;
3. Kushirikiana na BMT , Mashirikisho ya michezo ya kitaifa na kimataifa, ili kuendeleza michezo kwa ujumla katika Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Idara Maalum ya SMZ;
4. Kuhakikisha, ujenzi uboreshaji na matumizi ya miundombinu na vifaa vya michezo vinazingatia viwango vinavyokubaliwa kitaifa na kimataifa;
5. Kuendeleza ufundi, utaalam na kuanzisha Programu na vituo vya kuibua na kuinua vipaji vya wanamichezo kwa wanachama wake;
6. Kuandaa na kuendesha mashindano ya Michezo ya Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Idara Maalum za SMZ kila mwaka na kuwatayarisha wachezaji kwa mashindano ya kitaifa na kimataifa;
7. Kuhakikisha kwamba vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama pamoja na Idara Maalum za SMZ zinashiriki katika michezo iliyoandaliwa na BAMMATA;
8. Kuandaa, kutoa na kuratibu mafunzo kwa walimu, waamuzi na wachezaji, viongozi na wadau wa manufaa wa vyombo vya Ulinzi na Usalama na Idara Maalum za SMZ;
9. Kuendeleza na kudumisha Sera ya Taifa ya Michezo katika Majeshi ya Ulinzi na Usalama
10. Kuimarisha timu zilizomo ndani ya Kanda ya BAMMATA na kuunda timu mbalimbali kwa ajili ya michezo ya kitaifa na kimataifa;
11. Kufanya lolote ambalo halikutajwa katika madhumuni na shabaha hizi ambalo ni kwa manufaa ya maendeleo ya michezo ya Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Idara Maalum za SMZ Kitaifa na Kimataifa