Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe. Ali Abdulgulam Hussein, amekabidhi rasmi bendera ya Zanzibar kwa timu ya Netball ya KVZ wanawake kuelekea ushiriki wao katika Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki yatakayofanyika nchini Kenya.
Timu hiyo ya KVZ ni Mabingwa wa Zanzibar na Mabingwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msimu wa 2025/2026, jambo lililowapa nafasi ya kuiwakilisha Zanzibar na Tanzania katika mashindano hayo ya kikanda.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika Makao Makuu ya KVZ, Mtoni Mjini Zanzibar, Mhe. Hussein aliwataka wachezaji hao kuwa mabalozi wazuri wa Zanzibar kwa kuonesha nidhamu, mshikamano, uzalendo na ari ya ushindi wanapokuwa uwanjani. Aidha, alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono maendeleo ya michezo, hususan kwa timu za wanawake ambazo zimekuwa zikifanya vizuri na kuiletea nchi heshima katika mashindano mbalimbali.
Kwa upande wao, viongozi na wachezaji wa KVZ Netball wameahidi kupambana kwa nguvu zote ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kuendelea kuipeperusha vyema bendera ya Zanzibar na Tanzania katika mashindano hayo. Wamesema maandalizi yao yamekamilika na wana imani ya kufanya vizuri dhidi ya klabu nyingine zitakazoshiriki kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki.
Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki yanatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa kuzikutanisha timu bora kutoka ukanda huo, huku yakitoa fursa kwa wachezaji kuonesha uwezo wao, kupata uzoefu wa kimataifa na kuongeza ushindani katika mchezo wa netball.
📸 Timu ya KVZ Netball wanawake, Mabingwa wa Zanzibar na Mabingwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania msimu wa 2025/2026, wakiwa katika hafla ya kukabidhiwa bendera ya Zanzibar kuelekea Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki nchini Kenya
📸 Mhe. Ali Abdulgulam Hussein akimkabidhi bendera ya Zanzibar nahodha wa timu ya KVZ Netball wanawake ikiwa ni ishara ya kuwaaga na kuwatakia mafanikio katika mashindano hayo ya kikanda yatakayofanyika nchini Kenya.
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe. Ali Abdulgulam Hussein
Luteni Kanali Said A. Shamuhuna