MICHEZO YA MAJESHI (BAMMATA) YAFUNGULIWA RASMI MKOANI MWANZA

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Afungua Rasmi Mashindano ya BAMMATA 2026 Mwanza

MWANZA, SEPTEMBA 21, 2026: Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amefungua rasmi mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) 2026, yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza.

Mashindano hayo yanayowakutanisha wanamichezo kutoka katika Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutoka kanda saba nchini yataendelea hadi Oktoba 5, 2026, yakibeba kaulimbiu isemayo:

“Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kudumisha Amani.”

Kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa Watanzania, huku ikisisitiza umuhimu wa kila mmoja kushiriki katika kulinda na kudumisha amani na utulivu wa nchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, Mhe. Abdulla amesema dhamira ya BAMMATA si kuimarisha ushindani wa michezo pekee, bali pia kutumia michezo kama nyenzo ya kujenga umoja, mshikamano, urafiki na mahusiano mema miongoni mwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Amepongeza viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kuendelea kuthamini michezo kama nyenzo muhimu ya kujenga nidhamu, afya, upendo, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa watumishi.

Mhe. Abdulla ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa wazalendo na kushiriki katika kulinda tunu ya amani ya nchi, akieleza kuwa amani ni msingi muhimu wa ukuaji wa uchumi, maendeleo ya jamii, utalii na sekta nyingine zinazogusa maisha ya wananchi.

“Natoa wito kwa wananchi tuendelee kuwa wazalendo na kulinda tunu ya amani ya nchi yetu ili kukuza utalii na maendeleo ya sekta mbalimbali zinazogusa maisha ya watu wetu,” amesema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi na watumishi kuendelea kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora, akieleza kuwa afya bora ni mtaji muhimu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Akizungumzia mashindano hayo, Mhe. Abdulla amewataka wanamichezo na waamuzi kuzingatia kanuni na sheria za michezo, akisisitiza umuhimu wa mashindano kuwa jukwaa la kuonesha vipaji, nidhamu na uwezo wa kushindana kwa haki.

“Mashindano haya yanapaswa kuwa mahali pa kuonesha vipaji, nidhamu na uwezo wa kushindana kwa haki. Nawasihi washiriki na waamuzi kuzingatia kanuni na sheria,” amesema.

Michezo kama sehemu ya kujenga nidhamu na mshikamano

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Rhimo Nyansaho, amesema mashindano hayo yanaonesha namna Serikali inavyoupa umuhimu michezo katika kujenga afya, nidhamu, umoja na mshikamano miongoni mwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, CDF Jenerali Jacob Mkunda, amesema michezo ndani ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama si burudani pekee, bali ni sehemu muhimu ya maandalizi ya askari katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Michezo siyo burudani tu bali ni maandalizi ya askari katika kuimarisha ulinzi. Ndani ya jeshi sisi kwetu michezo ni sehemu ya kazi,” amesema.

Kanda saba kushiriki BAMMATA 2026

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa BAMMATA, Meja Jenerali Said Hamis Said, amesema mashindano hayo yameshirikisha wanamichezo kutoka kanda saba ambazo ni Ngome, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Magereza, Uhamiaji, Polisi, Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Kikosi Maalum cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Amesema washiriki watashindana katika michezo mbalimbali ikiwemo soka, mpira wa mikono, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, riadha, vishale, kulenga shabaha na netiboli.

Mashindano hayo yanatoa fursa kwa wanamichezo kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama kukutana, kushindana kwa kuzingatia kanuni za michezo na wakati huo huo kujenga mahusiano na mshikamano katika utekelezaji wa majukumu yao ya kitaifa.

Mwanza kunufaika na BAMMATA 2026

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. CP Salum Rashid Hamduni, amesema kufanyika kwa mashindano hayo mkoani Mwanza kumekuwa na manufaa mbalimbali kwa Mkoa, ikiwemo kuongeza fursa za burudani kwa wananchi, kuchochea mzunguko wa fedha, kuimarisha mshikamano na kukuza utalii wa michezo.

Mhe. Hamduni amesema uwepo wa washiriki na wageni mbalimbali kutoka maeneo tofauti nchini unatoa fursa kwa Mwanza kuendelea kujitangaza kupitia michezo na vivutio vyake vya utalii.

Aidha, ameomba Mkoa wa Mwanza upewe nafasi ya kuandaa tena mashindano hayo mwaka 2027, akieleza kuwa Mkoa una uwezo wa kuendelea kuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya michezo na shughuli nyingine zinazolenga kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

BAMMATA 2026: Michezo, Afya, Umoja na Amani

Mashindano ya BAMMATA 2026 yanaendelea kuwa jukwaa la kuunganisha wanamichezo kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama, kuibua na kukuza vipaji, kuimarisha afya na nidhamu, pamoja na kujenga mahusiano na mshikamano.

Kupitia kaulimbiu ya mwaka huu, “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kudumisha Amani,” BAMMATA 2026 inasisitiza umuhimu wa umoja na ushirikiano katika kulinda amani na utulivu wa nchi, sambamba na kutumia michezo kama nyenzo ya kujenga jamii yenye afya, mshikamano na mahusiano mema.

Mashindano ya BAMMATA 2026 yanaendelea katika Uwanja wa CCM Kirumba na maeneo mengine ya michezo mkoani Mwanza hadi Oktoba 5, 2026.

Matukio katika picha

Piya Pamoja ya Mgeni Rasmi akiwa na Kamati Tendaji ya BAMMATA

Piya Pamoja ya Mgeni Rasmi akiwa na Kamati Tendaji ya BAMMATA

Pichani Mgeni Rasmi wa Ufunguzi wa Mashindano ya BAMMATA 2026 akiwa na wageni Waalikwa wa vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mwanza

Pichani Mgeni Rasmi wa Ufunguzi wa Mashindano ya BAMMATA 2026 akiwa na wageni Waalikwa wa vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mwanza

Wageni Waalikwa kwenye Sherehe ya Ufunguzi wa Mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania mwaka 2026 mkoani Mwanza

Wageni Waalikwa kwenye Sherehe ya Ufunguzi wa Mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania mwaka 2026 mkoani Mwanza

Garide la Heshima la Ufunguzi likipita  Mbele ya Mgeni Rasmi

Garide la Heshima la Ufunguzi likipita Mbele ya Mgeni Rasmi